Nini kitakacho tokea Barani Ulaya baada ya kuangushwa Sarkozy?!
Matokeo ya uchaguzi nchini Ufaransa na Ugiriki yaleta wasiwasi EU
Wikiendi iliyopita, Wafaransa wamemchagua rais mpya, na nchini Ugiriki pia ulifanyika uchaguzi wa wabunge ambao ni wa kwanza kufanyika tangu nchi hiyo ikumbwe na msukosuko mkubwa wa madeni. Uchaguzi huo umeleta wasiwasi kwa wanasiasa wa Umoja wa Ulaya na viongozi wa nchi wanachama wa umoja huo kuhusu maendeleo ya kushughulikiwa msukosuko wa madeni.
Ujerumani ni nchi yenye wasiwasi mkubwa zaidi na matokeo haya ya uchaguzi wa rais nchini Ufaransa. Kwani katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili iliyopita toka msukosuko wa madeni uzikumbe Nchi za Ulaya, Ujerumani ilikuwa ikishirikiana na Ufaransa katika kutekeleza sera za kubana matumizi katika nchi za wanachama wa Umoja wa Ulaya. Ujerumani ina wasiwasi kwamba, kushindwa kupata awamu nyingine ya urais kwa Nicolas Sarkozy kutasababisha kuvunjika kwa ushirikiano huo kati ya Ufaransa na Ujerumani, na Nchi zengine za wanachama wa Umoja wa Ulaya zinaweza kupunguza nguvu ya kutekeleza sera za kubana matumizi na kuleta mageuzi ya kiuchumi, na hata kuziweka kando. Tumeshuhudia kuwa toka mwanzoni mwa mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulianza kurekebisha sera zake za kiuchumi, yaani kutoa kipaumbele kwa lengo la kuhimiza ongezeko la uchumi. Tangu msukosuko wa madeni utokee barani Ulaya, wanasiasa wa Umoja wa Ulaya walikuwa wanatatizwa na kuweka uwiano kati ya kubana matumizi na kuhimiza ongezeko la uchumi. Kutoka na matatizo ya madeni, nchi za Ulaya zililazimika kuchukua hatua za kubana matumizi, lakini pia zina wasiwasi kwamba hatua hizo zinaweza kukwamisha ongezeko la uchumi. Hivi sasa inaonekana wasiwasi huo umebadilika kuwa hali halisi. Kubana matumizi kupita kiasi kumefanya uchumi barani Ulaya urudi katika hali ya kudidimia na idadi ya watu wasio na ajira kuendelea kuongezeka. Umoja wa Ulaya unatunga mkakati wa kuchochea ongezeko la uchumi ambao unatarajiwa kupitishwa kwenye mkutano wa wakuu utakaofanyika mwezi Juni. Hata hivyo Ujerumani haifurahii maoni hayo na haipendi sera za sasa za kubana matumizi ziachwe.